MULEHI: USHIRIKIANO WA IDARA MBALI MBALI UNAHITAJIKA KATIKA KUSHUGHULIKIA MAJANGA KWENYE SERIKALI ZA KAUNTI.
Wadau kutoka sekta mbali mbali katika serikali za kaunti pamoja na vyombo vya habari wamekongamana mjini Kericho kupokea mafunzo kuhusiana na jinsi ya kuripoti na kushughulikia majanga yanayotokana na hali mbali mbali.
Akizungumza katika mahojiano na wanahabari mkufunzi katika kongamano hilo Patrick Mulehi, amesema kwamba lengo kuu la kongamano hilo ni kuhakikisha idara mbali mbali za serikali zinafahamu jinsi ya kushirikiana katika kukabili majanga yanapotokea.
“Wakati wa majanga watu huwa wanachanganyikiwa, na unapata kwamba kuna mashirika mengi ambayo huhusika wakati huo, lakini kwa kufanya kazi kwa pamoja inapelekea kazi kuwa rahisi. Na ndio maana tumekongamana hapa ili tuweze kufahamu jinsi ambavyo tutashirikiana hasa wakati wa majanga.” Alisema Mulehi.
Mulehi ambaye pia anahudumu na shirika la habari la BBC eneo la kaskazini mwa bonde la ufa alielezea matumani kwamba kongamano hilo litaleta utofauti mkubwa wa jinsi ambavyo majanga yatashughulikiwa tofauti na jinsi ilivyokuwa awali.
“Matumaini yangu kama mkufunzi ni kwamba tutakapotoka hapa tutaona matunda bora itakapofika wakati wa kushughulikia majanga mbali mbali.” Alisema.
Afisa katika shirika la msalaba mwekundu kaunti ya Pokot magharibi Cyrus Mutai alitumia fursa hiyo kuelezea mikakati ambayo shirika hilo limeweka kukabili aina yoyote ya majanga ambayo huenda yakatokea hasa wakati huu ambapo mvua ya Elnino inatarajiwa kushuhudiwa nchini.
“Sisi kama msalaba mwekundu tuna kitengo ambacho kimepokea mafunzo na kiko tayari kushughulikia hali mbali mbali ambazop huenda zikashuhudiwa wakati wa majanga. Pia tumeweka mipango ambayo itatusaidia kufahamu kile ambacho tutapasa kufanya wakati hali ikitokea.” Alisema Mutai.
Kwa upande wake afisa katika idara ya afya kaunti ya Pokot magharibi Josephine Arusio alielezea umuhimu wa kongamano hilo alilosema kwamba litaimarisha utendakazi wa idara ya afya kupitia ushirikiano baina ya idara hiyo na wadau ikiwemo wanahabari, na shirika la msalaba mwekundu.
“Ni jambo la muhimu tukishirikiana sisi kama idara ya afya, vyombo vya habari na shirika la msalaba mwekundu ili kuimarisha utendakazi wetu.” Alisema Arusio.