MUKENYANG ATAJA JUHUDI ZA KUMBANDUA AFISINI KUWA ZILIZOCHOCHEWA KISIASA.


Spika wa bunge la kaunti hii ya pokot magharibi Catherine Mukenyang akitarajiwa kufika mbele ya kamati ya bunge hilo kujitetea baada ya kuanzishwa mchakato wa kumbandua afisini, amewalaumu pakubwa mahasimu wake wa kisiasa kwa masaibu yanayomkumba.
Mukenyang ameitaja hoja ya kutaka kumbandua iliyowasilishwa na mwakilishi wadi ya Endough Evanson Lomaduny kuwa iliyochochewa kisiasa huku akidai kuwa wapo baadhi ya waakilishi wadi ambao wamekiri kushurutishwa na baadhi ya viongozi kaunti hii ya Pokot magharibi kutia saini ya kubanduliwa kwake afisini.
Amesema kuwa masaibu yake yametokana na juhudi zake kutetea raslimali za umma akidai kuwepo ushahidi wa kutosha unaodhihirisha matumizi mabaya ya fedha za umma na uongozi wa serikali ya kaunti hii hasa fedha za basari akisema yuko tayari kumenyana na walio kinyume naye.
Wakati uo huo Munkenyang amesema kuwa hatua hiyo haitaathiri mikakati yake ya kugombea kiti cha mwakilishi kina mama kaunti hii katika uchaguzi mkuu ujao huku akiwataka wafuasi wake kusalia watulivu wakati sheria ikichukua mkondo wake.
Ikumbukwe hii si mara ya kwanza kwa bunge hilo kujaribu kumbandua afisini spika mukenyang jaribio la kwanza likiwa mwaka jana.