MUKENYANG AELEKEA MAHAKAMANI KUPINGA KUBANDULIWA AFISINI.


Aliyekuwa spika wa bunge la kaunti hii ya Pokot magharibi Catherine Mukenyang amewalaumu wabunge katika bunge hilo kwa hatua ya kumbandua afisini bila ya kumpa nafasi ya kujitetea ndhidi ya tuhuma ambazo ziliibuliwa dhidi yake.
Akizungumza baada ya zaidi ya waakilishi wadi 20 kuunga mkono hoja ya kuondolewa kwake kama spika, Mukenyang amesema licha ya juhudi zake kulitaka bunge hilo kumpa muda wa siku 7 kutafuta ushahidi wa kutosha kujitetea bunge hilo lilidinda kumsikiliza na badala yake kumbandua.
Wakili wake Mukenyang Eric Naibei aidha ameshutumu bunge hilo kwa kile amedai limekiuka haki ya mteja wake kwa kumnyima nafasi ya kusikilizwa, akidokeza kuwa wanaelekea mahakamani kupinga uamuzi huo wa bunge.
Kwa upande wao waakilishi wadi waliopinga hoja hiyo wakiongozwa na mwakilishi wadi maalum Elijah Kasheusheu wamesema kuwa hatua ya kumbandua Mukenyang afisini imechochewa kisiasa kwa nia ya kuwanyima kina mama nafasi za uongozi.