MUKENYANG ABANDULIWA KAMA SPIKA WA BUNGE LA POKOT MAGHARIBI
Spika wa bunge la kaunti ya Pokot magharibi Catherine Mukenyang hatimaye ameondolewa afisini.
Hii ni baada ya idadi kubwa ya wabunge katika bunge hilo kuunga mkono hoja ya kumwondoa afisini iliyowasilishwa na mwakilishi wadi ya Endough Evanson Lomaduny.
Mukenyang ametimuliwa baada ya wakilishi wadi 25 kupiga kura ya ndio huku 7 wakipinga hoja hiyo.
Wengi wa wabunge katika bunge hilo ambao waliunga mkono hoja ya kuondolewa spika Mukenyang wamemlaumu spika huyo kwa matumizi mabaya ya afisi na kukiuka sheria katika maamuzi mengi ambayo alikuwa kifanya.
Awali ombi la spika huyo katika vikao hivyo kutaka kupewa muda zaidi kujibu tuhuma dhidi yake lilikataliwa na spika wa muda ambaye amesema kuwa Mukenyang alikuwa na muda wa kutosha kufanya hivyo baada ya kupewa awali siku saba.
Hata hivyo Mukenyanga alidinda kujibu idadi kubwa ya maswali ambayo aliulizwa na wabunge katika bunge la kaunti hii akidai kutopewa ushahidi wa tuhuma dhidi yake.
Alilazimika kuondoka kabla ya kumalizika vikao baada ya wakili wake kuomba nafasi hiyo ili kumwona daktari kutoka na maswala ya kiafya.