MTU MMOJA AULIWA KUFUATIA UVAMIZI TILAKAI POKOT MAGHARIBI.


Mtu mmoja ameuliwa huku wengine watatu wakiuguza majeraha mabaya baada ya shambulizi lililotokea katika vijiji vya Tilakai, Chepkokogh na Cheratak kwenye Wadi ya Lomut Pokot Magharibi.
Uvamizi huo umetekelezwa na majambazi wanaoaminika kutoka katika Kaunti ya Elgeyo Marakwet ambapo idadi ya mifugo isiyojulikana imeibwa na wahalifu hao.
Inadaiwa wakazi wengi wa mipakani mwa Kaunti za Pokot na Marakwet wanamiliki silaha haramu ambazo wanazitumia katika kuendeleza uvamizi.
Uvamizi huo umetokea wiki moja baada ya watoto wawili wakazi wa Kaunti ya Pokot Magharibi kufariki dunia baada ya kuvamiwa na majambazi wanaoaminika kutoka katika Kaunti ya Turkana huku serikali ikikosa kuingilia kati suala hilo zima.
Imedhihirika wazi kwamba mashambulizi baina ya jamii za wafugaji yameongezeka wakati huu wa ukame kiasi cha kulemaza shughuli za masomo katika maeneo ya Baringo.
Wiki iliyopita Mwalimu mmoja aliripotiwa kuuliwa katika Kaunti ya Baringo saa chache tu baada ya kumaliza mafunzo shuleni ambapo alikuwa anarejelea makazi yake.