MTU MMOJA AULIWA KATIKA UVAMIZI CHESOGON.


Taharuki imetanda eneo la Lebei Chesogon mpakani pa kaunti hii ya pokot magharibi na Elgeyo marakwet baada ya mtu mmoja kuuliwa na mwingine kujeruhiwa vibaya usiku wa kuamkia leo baada ya wavamizi wanaoaminika kuwa wezi wa mifugo kuvamia eneo hilo.
Akithibitisha hilo naibu kamishina eneo la Sigor Were Simiyu amesema kisa hicho kinaaminika kuwa cha kulipiza kisasi baada ya mkazi mmoja wa pande husika kuuliwa juma moja lililopita na wavamizi wanaoaminika kutoka kaunti jirani.
Ni kauli ambayo imekaririwa na chifu wa eneo hilo James Kapewon ambaye amesema kuwa zaidi ya ng’ombe 10 walikuwa wameibwa eneo hilo jumatatu juma hili hali ambayo ilichochea tukio hilo.
Ni kisa ambacho kimekashifiwa vikali na seneta wa kaunti hii ya pokot magharibi Samwel Poghisio ambaye ameelezea haja ya swala la usalama kanda hii kushughulikiwa kwa dharura.