MTU MMOJA AUAWA KATIKA UVAMIZI SAMARICH.

Taharuki imetanda katika kijiji cha Uncertainty Sarimach mpakani pa kaunti hii ya Pokot magharibi na kaunti jirani ya Turkana baada ya mtu mmoja kufariki, na wengine kadhaa kujeruhiwa vibaya na mamia ya mifugo kutoroshwa na majangili wanaoshukiwa kutoka kaunti jirani ya Turkana.
Wavamizi hao wanaripotiwa kuwavamia wachungaji katika eneo la malisho karibu na mto Malmalta kwenye mpaka wa kaunti hizi mbili.
Gavana wa kaunti ya Pokot Magharibi John Lonyangapuo ambaye alizuru majeruhi katika hospitali ya Kapenguria amekashifu vikali tukio hilo akivitaka vyombo vya usalama kuimarisha usalama eneo hilo la mpakani.
Lonyangapuo Amesema kuwa kuna utepetevu kati ya maafisa wa usalama wanaohudumu katika eneo hilo akitoa wito kwa serikali kurejesha askari wa akiba pamoja na kuwapokonya wakazi silaha katika eneo hilo.
Naibu wa kamishina katika kaunti ndogo ya Pokot ya kati Jeremiah Koech Tumo ambaye alidhibitisha kisa hicho amesema kuwa maafisa wa usalama wametumwa katika eneo hilo kutuliza hali.