MTU MMOJA AUAWA HUKU WAWILI WAKIJERUHIWA TURKWEL.

Mtu mmoja ameuliwa kwa kupigwa risasi huku wengine wawili wakiachwa na majeraha mabaya eneo la Turkwel kaunti ya Pokot magharibi katika shambulizi la hivi punde ambalo linaaminika kutekelezwa na wahalifu wanaoshukiwa kutoka kaunti jirani.

Kulingana na walioshuhudia kisa hicho cha jumanne jioni, tatu hao walikuwa kwenye pikipiki wakitoka eneo la Sigor kuelekea Turkwel kabla ya kuvamiwa eneo la Sarmach ambapo dereva wa pikipiki hiyo aliuliwa papo hapo huku abiria wawili waliokuwa wamebebwa wakinusurika na majeraha mabaya.

“Hawa watu watatu walikuwa wanatoka Sigor wakiwa kwenye pikipiki. Walipofika eneo la Sarmach wavamizi kutoka kaunti jirani wakaanza kuwashambulia kwa risasi ambapo dereva wa pikipiki aliuawa papo hapo huku wawili wakinusurika na majeraha, na sasa wanaendelea kutibiwa katika hospitali moja eneo hili.”  Alisema Philip Korinyang mkazi wa Turkwel ambaye alishuhudia kisa hicho.

Alitoa wito kwa idara za usalama kuimarisha usalama eneo hilo huku pia akiwalaumu viongozi wa kisiasa kwa kile alidai wanachochea hali ya utovu wa usalama maeneo hayo ya mipakani kufuatia matamshi ya uchochezi ambayo wanatoa katika mikutano ya umma.

“Viongozi wa siasa wanafaa kuwa makini na maneno ambayo wanatumia kwenye mikutano ya umma. Jana tulipata ripoti kwamba kiongozi mmoja kutoka kaunti jirani alikuwa akiwachochea wananchi kwamba watege watu kutoka kaunti hi barabarani.” Alidai Korinyang.