MSWADA WA MAREKEBISHO YA SHERIA ZA UCHAGUZI WAENDELEA KUIBUA HISIA NCHINI.


Viongozi mbali mbali wa kisiasa nchini wameendelea kupinga mswada wa marekebisho kuhusu sheria za uchaguzi ambao tayari umewasilishwa bungeni na kiongozi wa wengi katika bunge la kitaifa Amos Kimunya.
Wa hivi punde kutolea hisia mswada huo ni aliyekuwa mwakilishi wadi maalum Lucy Lotee ambaye amedai kuwa mipango ya kufanyia marekebisho sheria za uchaguzi inalenga kutoa mianya ya wizi wa kura katika uchaguzi mkuu ujao.
Wakati uo huo Lotee ambaye pia ametangaza nia ya kugombea kiti cha mwakilishi wadi ya Kapenguria kaunti hii ya Pokot magharibi amesema kuwa atatoa kipau mbele kwa maswala yanayohusu vijana na kina mama iwapo atatwaa wadhifa huo.
Aidha Bi. Lotee ameshutumu mwakilishi wadi wa sasa Emmanuel Madi akisema kuwa amefeli kutekeleza miradi ya maendeleo katika kipindi ambacho amekuwa akihudumu huku akiwataka wakazi katika wadi hii kufanya uamuzi wa busara katika uchaguzi mkuu ujao.