MSWADA WA MAREKEBISHO YA KATIBA WAENDELEA KUKOSOLEWA


Hisia mseto zimeendelea kutolewa na viongozi mbali mbali katika kaunti hii ya Pokot magharibi kuhusu hatma ya mswada wa marekebisho ya katiba BBI, wa hivi punde kuzungumzia hilo akiwa mbunge wa Kapunguria Samwel Moroto ambaye ameelezea haja ya kutekelezwa kikamilifu katiba ya mwaka 2010 kwanza kabla ya kuanza kufikiria kuifanyia marekebisho.
Akizungumza na wanahabari mbunge wa Kapenguria samwel moroto amesema kuwa katiba ya mwaka 2010 ambayo ilikuwa ya manufaa makubwa kwa taifa haijatekelezwa kikamilifu na sasa hamna haja ya kuanza kuifanyia marekebisho.

Moroto amepuuzilia mbali madai kuwa Mpango wa upatanishi BBI utapelekea utulivu wa kisiasa nchini na kukomesha machafuko ya kila baada ya uchaguzi mkuu akisema machafuko hayo husababishwa na wanasiasa wenyewe.

Aidha ameshutumu kile amedai kulazimishwa mabunge ya kaunti kupitisha mswada wa marekebisho ya katiba ambao baadaye umegundulika kuwa usio halisi, elezea haja ya wananchi kupewa uhuru wa kutoa maoni yao.