MSHUKIWA WA MAUAJI AJIWASILISHA KITUO CHA POLISI KAPENGURIA.


Maafisa wa upelelezi katika kituo cha polisi cha kapenguria kaunti hii ya pokot magharibi wanatarajiwa kumfungulia mashtaka ya mauaji jamaa mmoja ambaye amejiwasilisha jana katika kituo hicho akidai kumuua mpenziwe.
Inaarifiwa Nelson baraza mwenye umri wa miaka 29 alijiwasilisha katika kituo hicho cha polisi akitaka kumwona mkurugenzi wa idara ya upelelezi katika kituo hicho ili kuripoti mauaji hayo ambayo anadaiwa kuyatekeleza.
Kulingana na taarifa kutoka idara hiyo kwa vyombo vya habari, mshukiwa aliandamana na maafisa wa polisi hadi eneo la kamatira ambako aliutupa mwili huo wa mwenda zake.
Baada ya kudadisiwa zaidi na maafisa wa polisi Baraza anadaiwa kutoa ushahidi wote kuhusu kitendo hicho huku akidai kuwa alilazimika kumuua mpenziwe kutokana na uchungu baada ya kugundua kuwa alikuwa na mpenzi mwingine kando naye.
Maafisa wa upelelezi walikagua eneo la tukio ambako ulipatikana mwili wa marehemu anayekisiwa kuwa mwenye umri wa miaka 20 na kupata kitambaa kilichotumika kumuua na kisha kumkamata mshukiwa ambaye alikiri kutekeleza mauaji hayo.