MSAKO DHIDI YA WANAOMILIKI BUNDUKI WAENDELEZWA UGANDA, WATU 26 KUTOKA JAMII YA POKOT WAKIZUILIWA NA POLISI.

Takriban watu 26 kutoka jamii ya pokot wanaoishi nchini Uganda wanazuiliwa katika kituo cha polisi cha Nakapirpirit kwa tuhuma za uvamizi kwa kutumia bunduki.

Msako dhidi ya wanaomiliki bunduki unaoendelezwa kwa siku ya nne sasa umeshinikizwa na serikali ya rais Yoweri Museveni baada ya majambazi wanaokisiwa kutoja jamii ya Pokot kuvamia jamii jirani ya Karamoja.

Msako huo pia umeendelezwa katika jamii ya Karamoja kufuatia uvamizi wa mara kwa mara baina yao na jamii ya Pokot.

Hata hivyo msako huo ambao huendelezwa nyakati za usiku umekosolewa vikali na wakazi wakiongozwa na Christopher Lotudo, mkazi wa kijiji cha Abong’ai, wakisema umewasababishia mahangaiko kina mama na watoto ambao wamelazimika kukesha msituni kwa kuhofia usalama wao.

“Oparesheni imeendelezwa maeneo haya tangu ijumaa usiku ambapo kufikia sasa watu 26 wamekamatwa ambapo inadaiwa watu kutoka jamii ya Pokot walivamia karamojong. sasa watu wanaishi kwa hofu, kina mama na watoto wanalala msituni na hakuna shughuli ambazo zinaendelea eneo hili.” Alisema Lotudo.

Alisema kwamba serikali inapasa kutumia njia mbadala ya kuwatafuta wahalifu badala ya kuvuruga amani ya watu wasio na hatia.

Alipendekeza viongozi wote wa jamii hizo kufanya kikao cha kushughulikia tatizo hilo na hata kuwataja waziwazi wanaoshukiwa kuhusika uhalifu huo bila ya kuwaficha.

“Serikali inafaa kutumia wazee kutoka jamii zote mbili. Wafanye mkutano ambapo watawataja hadharani majina ya watu ambao wanaendeleza uvamizi kuliko kutumia njia ya sasa ambayo inaumiza raia.” Alisema.

Hata hivyo inadaiwa kwamba oparesheni inayoendelea kwa sasa imekumbwa na ufisadi mwingi, ambapo kabla ya mshukiwa kuachiliwa anafaa kutoa shilingi elfu tano pesa za Kenya badala ya bunduki.