MRENGO WA RUTO WALALAMIKIA SHERIA TATA ZA VYAMA VYA KISIASA.


Wabunge kwenye eneo la bonde la ufa wanaoegemea mrengo wa naibu rais Dkt William Ruto wameendelea kutoa kauli mseto kuhusu sheria tata ya vyama vya kisiasa iliyotiwa saini na rais Uhuru Kenyatta na kuwa sheria juma lililopita.
Mbunge wa Keiyo kusini katika kaunti ya Elgeiyo marakwet Daniel Rono anasema kuwa sheria hiyo kwa upande mmoja itakandamiza chama cha uda ambacho ni kipya na bado hakijakuwa na sajili rasmi ya wanachama wake.
Kwenye kikao na wanahabari mjini Eldoret Rono amesema kuwa kulingana na sheria hiyo wanachama wa chama cha kisiasa watakaotambuliwa ni wale walio kwenye orodha ya msajili wa vyama na ambapo huenda wafuasi wa uda majina yao bado hayajaondolewa kwenye sajili ya vyama vingine.
Hata hivyo Rono amesema kuwa sheria hiyo itaufaa mrengo wao kwani watakuwa na uwezo wa kubuni muugano na kuwa na ushirikiano na vyama vingine vya kisiasa kando na ANC na Ford kenya kabla ya tarehe 9 mwezi aprili.
Aidha Rono amesema kuwa kama viongozi huwenda wakalazimika kuwasilisha kesi mahakamani ya kutaka kusitishwa utekelezaji wa sheria hizo hadi wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2027.