MRADI WA UNYUNYIZIAJI MAJI MASHAMBA WA PARASANY WAKAMILIKA.
Shirika la SEFA limekabidhi rasmi mradi wa unyunyiziaji maji mashamba wa parasanyi ambao umetelezwa chini ya mpango wa ustahimilivu kwa usimamizi wa serikali ya kaunti hii.
Akizungumza katika hafla ya kukabidhi usimamizi wa mradi huo kwa serikali ya kaunti, mkurugenzi wa mradi huo Rebecca Chebet amesema kuwa zaidi ya wakazi 200 wanalengwa katika mradi husika ambao aidha unalenga kutimiza moja ya ajenda nne za serikali ya utoshelezaji wa chakula.
“Leo tunapeana mradi huu kwa serikali ya kaunti hii ambayo ni mshikadau mkuu ambaye amekuwa akituunga mkono kikamilifu. Kuanzia leo ni serikali ndiyo itashikilia jamii kuhakikisha mradi huu unafanikishwa ili wakazi wapate chakula.” Alisema.
Kennedy Gakinya ambaye ni mhandisi katika mradi huo unaotekelezwa eneo la Seker ametoa wito kwa wadau hasa serikali ya kaunti hii kutoa msaada kwa wakulima ili kuhakikisha kwamba mradi huo unaendelea kuimarika na kuwanufaisha zaidi wakazi wa eneo hilo.
“Wadau wakiongozwa na serikali ya kaunti wawasaidie wakulima kwa kuwapa mbegu, kutoa mafunzo kwa wakulima na hata kutafuta soko kwa ajili ya mazao yao kwa kuwa yatakuwa mengi.” Alisema.
Gakinya aliongeza kwa kusema kuwa, “wakulima hawapasi kuachwa pekee kujitegemea katika mradi huu, serikali inapasa kuhakikisha kwamba hautafeli.”
Wakazi wa eneo hilo wakiongozwa na Joakim Malemusia wamepongeza shirika hilo kwa kuanzisha mradi huo wa ekari 80 wanaosema kuwa utawafaa zaidi kwa kutoa suluhu kwa uhaba wa chakula hasa nyakati za ukame.
“Kabla hatujakuja kwenye mradi huu, tulikuwa tukitumia mbinu ya kunyunyizia maji kwa kutumia mikondo ya maji ambayo ilianzishwa mwaka wa 1873. Mbinu hii haikutosheleza mahitaji yetu ya maji ila sasa mradi huu unatosheleza mahitaji yetu.” Walisema.