MPANGO WA KUTOA VISODO KWA WANAFUNZI WAZINDULIWA POKOT MAGHARIBI


Idadi kubwa ya wanafunzi wa kike kaunti hii ya Pokot magharibi hulazimika kusitisha masomo yao kutokana na unyanyapaa unaotokana na hadhi.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa zoezi la kutoa visodo kwa wanafunzi wa kike wa mbali mbali uliofanyika katika shule ya upili ya St Marys Siyoi, mhasisi wa shirika la Pendo Afrika faith Tanui aidha amesema kuwa mimba za mapema ambazo zinashuhudiwa kaunti hii hutokana na hali kuwa wanafunzi wengi hawana uwezo wa kupata visodo hali inayowalazimu kuingia katika mtego wa wanaume wanaoahidi kuwanunulia visodo hivyo.
Amesema hatua ya shirika hilo kutoa visodo kwa wanafunzi itawawezesha kusalia shule hata wanapokuwa katika hedhi kauli ambayo imesisitizwa na afisa mkuu mtendaji wa shirika la Padmad ambalo ni mshirika katika mpango huo Mathy Delao.
Mshirikishi wa elimu ya watu wenye mahitaji maalum kaunti hii ya pokot magharibi Lydia Agesa amesema kwa miaka mingi mtoto wa kike amekuwa akidhalilika kutokana na hedhi akisema mpango huu utawafaa zaidi wanafunzi hao, na kuwa japo wizara ya elimu ina mpango huo kwenye shule, hautoshelezi mahitaji ya wanafunzi akitaka wadau zaidi kujitokeza.
Mwalimu mkuu wa shule hiyo Wyclife Ngachi amepongeza mashirika hayo kwa kutoa kipau mbele kwa elimu ya mtoto wa kike, akitoa wito kwa wahisani zaidi kujitokeza na kuendeleza mpango huo kwa shule mbali mbali kaunti hii ya pokot magharibi.