MOTO WATEKETEZA SOKO LA MAKUTANO POKOT MAGHARIBI.


Mgombea ugavana wa kaunti hii ya Pokot magharibi kupitia chama cha UDA Simon Kachapin ameisuta vikali serikali ya gavana John Lonyangapuo kwa kile amesema kuwa utepetevu katika kushughulikia majanga kaunti hii.
Akirejelea mkasa wa moto ambao uliteketeza bidhaa za wafanyibiashara katika soko la makutano jumapili, Kachapin amedai kuwa licha ya kuwa utawala wake ulinunua gari la zimamoto, serikali ya sasa imehakikisha kwamba gari hilo halihudumu wakazi wakiathirika.
Aidha Kachapin amesema kuwa kaunti hii inahitaji mabadiliko ya uongozi kwani imekuwa katika hali mbaya tangu alipoondoka uongozini kama gavana wa kwanza, miradi aliyoanzisha ikitelekezwa na gavana wa sasa.
Wafanyibiashara katika soko la makutano kaunti hii ya Pokot magharibi hasa wa makaa walidai kukadiria hasara ya mamilioni ya fedha baada ya moto kuteketeza sehemu wanakoendelezea shughuli zao

Inakisiwa huenda mkasa huo ulisababishwa na hitilafu katika mfumo wa umeme.

Wameitaka serikali ya kaunti kuingilia kati kuwasaidia kwani wengi wao walikuwa wamechukua mikopo kuendeleza biashara zao na sasa wamesalia njia panda kufuatia mkasa huo ambao umewasababishia hasara kubwa.

Wafanyibiashara hao wameelezea kusikitishwa na hali kuwa kaunti hii inalazimika kutegemea gari la zimamoto kutoka kaunti ya Trans nzoia kufuatia madai ya kuharibika gari hilo la kaunti hii baada ya kuhusika ajali takriban miezi miwili iliyopita.