MOROTO ATANGAZA KUANGAZIA UHABA WA MADARASA KABLA KUJENGA MAABARA KATIKA SHULE ZA JUNIOR SECONDARY.
Mbunge wa kapenguria katika kaunti ya Pokot magharibi Samwel Moroto amesema kwamba atatoa kipau mbele kwa ujenzi wa madarasa katika shule ya msingi ya Talau ili kutoa nafasi ya kutosha kwa wanafunzi wa sekondari ya msingi kuendeleza shughuli zao za masomo sawa na wanafunzi wengine wa shule hiyo.
Akizungumza wakati alipoikabidhi shule ya upili ya Talau hundi ya shilingi alfu 700 ya pesa za basari kutoka hazina ya ustawishaji maeneo bunge NGCDF eneo bunge lake, Moroto alisema kwamba fedha ambazo zinatolewa na serikali kwa ajili ya wanafunzi hao wa sekondari ya msingi zitatumika kujenga madarasa.
Alisema kwamba uongozi wake utaimarisha maabara ya shule ya upili ya Talau ili wanafunzi hao wa sekondari ya msingi waitumie katika masomo yao ya utendaji.
“Waziri wa elimu alipokuja Tartar alisema kuna shilingi alfu 15,000 kwa kila mtoto na kwamba kati ya fedha hizo alfu 4 zitatumika kujenga maabara. Sisi tunataka kujenga kwanza madarasa. Kwa sasa tutaimarisha maabara ya shule ya upili ya Talau ili wanafunzi wa gredi ya 7 pia waitumie katika masomo yao ya utendaji.” Alisema Moroto.
Kulingana na mwalimu mkuu wa shule ya msingi ya Talau Barnabas Chirchir, wanakabiliwa na changamoto ya kutekeleza masomo ya wanafunzi hao wa sekondari ya msingi kutokana na changamoto ya uhaba wa walimu, vitabu na madarasa miongoni mwa mahitaji mengine muhimu.
“Hatuna vitabu vya kutosha vya kutumia kuwafunza watoto hawa. Naona kwamba tulikosa maandalizi ya kutosha kwa ajili ya kundi hili, kwa sababu hata walimu wanaofaa kuwahudumia bado hawapo.” Alisema Chirchir.