MOROTO ATAKA SERIKALI YA KENYA KWANZA KUPEWA MUDA WA KUREKEBISHA MAKOSA YALIYOSABABISHWA NA SERIKALI ILIYOTANGULIA.

Mbunge wa Kapenguria katika kaunti ya Pokot magharibi Samwel Moroto ametofautiana na ripoti za hivi karibuni kwamba taifa haliekei kwenye mkondo bora.

Akizungumza na wanahabari, Moroto alisema kwamba rais William Ruto anafanya kila juhudi kuhakikisha kwamba taifa linakuwa sawa kutokana na makosa ambayo yalisababishwa na uongozi uliotangulia na anapasa kupewa nafasi ya kutekeleza majukumu yake.

Moroto alisema rais anaendelea kutekeleza manifesto yake jinsi alivyoahidi wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu uliopita hasa kwa kuzingatia mkenya wa hali ya chini maarufu bottom up economic model.

“Taifa liko kwenye mkondo sahihi, na ni maombi yangu kwamba tumpe rais william Ruto nafasi apange serikali yake na awahudumie wananchi kikamilifu kulingana na manifesto yake ambayo inalenga kuwaangazia zaidi wananchi wa hali ya chini.” Alisema Moroto 

Aidha Moroto alidai kwamba baadhi ya viongozi ambao wanashutumu utendakazi wa rais Ruto ni wale ambao walinufaika na uongozi uliotangulia, na sasa nia yao ni kuhakikisha mwananchi wa kawaida hanufaiki na huduma za serikali ya Kenya kwanza.

“Kuna watu ambao hata watoto wao hawasomi hapa Kenya. Hao ndio walionufaika na serikali iliyotangulia na ndio wanaleta shida. Lengo lao hawataki mwananchi wa kawaida anufaike na huduma za serikali ya sasa ambayo ndio serikali ya mwananchi wa chini.” Alisema.