MOROTO ATAKA SERIKALI YA KAUNTI KUIMARISHA HOSPITALI ZA MAENEO YA MASHINANI.

Mbunge wa Kapenguria Samwel Moroto.

Na Benson Aswani.

Mbunge wa Kapenguria katika kaunti ya Pokot magharibi Samwel Moroto ametoa wito kwa serikali ya kaunti chini ya gavana Simon Kachapin kuhakikisha kwamba hospitali na vituo vya afya vinavyopatikana maeneo ambako kuna matatizo ya usafiri vinapata magari ya ambulansi.

Akiomboleza kifo cha afisa katika afisi ya CDF eneo bunge la Kapenguria, ambaye alikuwa anahudumu eneo la Turkwel, Moroto alisema kwamba ukosefu wa magari hayo umeathiri pakubwa huduma za hospitali hizo kwa wagonjwa.

Moroto alisema kifo cha afisa huyo kingeweza kuzuiliwa iwapo kungekuwa na gari la kumsafirisha hadi hospitali ya rufaa ya Kapenguria, kwani ugonjwa uliopelekea kifo chake ungeweza kutibiwa.

“Namhimiza gavana wa kaunti hii ya Pokot magharibi kwamba, ahakikishe hospitali zilizo maeneo ambako kuna matatizo ya usafiri zinapata magari ya ambulansi ya kusafirisha wagonjwa wanaohitaji matibabu zaidi, kwa sababu baadhi ya watu wanaaga dunia kutokana na magonjwa ambayo yanaweza kutibiwa.” Alisema Moroto.

Wakati uo huo Moroto alitoa wito kwa serikali ya gavana Kachapin kuimarisha vituo vya afya vilivyo maeneo ya mashinani kwa kuhakikisha kwamba vina dawa za kutosha pamoja na vifaa vingine vya matibabu ili kuimarisha huduma za matibabu kwa wananchi walio mbali na hospitali ya Kapenguria.

“Pia serikali ya kaunti ihakikishe kwamba hospitali zilizo maeneo hasa ya mashinani zinakuwa na dawa pamoja na maafisa wa afya wa kutosha. Tunajua kwamba serikali ya kaunti imejaribu lakini inapasa kufanya zaidi ili kuwaokoa watu wetu.” Alisema.