MOROTO ASHINIKIZA HAKI KWA WAKAZI WALIOFURUSHWA KWENYE ARDHI YA CHEPCHOINA.

Mbunge wa Kapenguria kaunti ya Pokot magharibi Samwel Moroto ameendelea kushutumu hatua ya kufurushwa wakazi wanaoishi katika ardhi yenye utata ya chepchoina mpakani pa kaunti hiyoi na kaunti jirani ya Trans nzoia.

Akizungumza katika hafla moja eneo hilo Moroto alisema kwamba inasikitisha kuona wakazi waliokabidhiwa vipande vya ardhi kwa njia ya halali kwenye ardhi hiyo na aliyekuwa rais hayati Daniel Moi, wakilazimika sasa kuishi kama wakimbizi katika ardhi zao wenyewe.

Kauli yake Moroto ilisisitizwa na mwakilishi kina mama kaunti hiyo Rael Kasiwai ambaye aliitaka serikali kupitia wizara ya ardhi kuchukua hatua za kuhakikisha kwamba waathiriwa wanashughulikiwa.

“Hawa wakazi walipewa vipande vya ardhi eneo hili na aliyekuwa rais hayati Daniel Moi, na wako hapa kwa njia ya halali. Lakini sasa watu fulani walikuja na kuwafurusha kwa ardhi zao na sasa wanaishi katika mazingira ambayo ni hatari kwao na hasa watoto.” Walisema.

Wakazi wa ardhi hiyo ambao waliathirika wameelezea masaibu wanayopitia katika makazi ya muda ambayo wanaishi kwa sasa wakitaka serikali kuhakikisha kwamba wanapata haki yao wanayostahili.

“Tunamwomba rais William Ruto aje hapa kushughulikia hali hii kwa sababu sisi tumehangaika sana. Tunalazimika kuishi kwenye nyumba za makaratasi na sasa wakati huu mvua inapoendelea kushuhudiwa tunahangaika sana.” Walisema waathiriwa.