MOROTO AKANA KUKINZANA KIMAJUKUMU NA GAVANA LONYANGAPUO.

Na Benson Aswani
Mbunge wa Kapenguria kaunti hii ya Pokot magharibi Samwel Moroto amekanusha madai ya kuwepo mkinzano wa kimajukumu kati yake na gavana wa kaunti hii John Lonyangapuo hasa katika maendeleo yanayuhusu ujenzi wa barabara eneo bunge la Kapenguria.
Hii ni baada ya hisia zilizoibuliwa na baadhi ya viongozi wa kaunti hii wakiongozwa na mwakilishi wadi ya Kapenguria Emmanuel Madi na wakazi kufuatia hatua ya kila mmoja wa wawili hao kuahidi kujenga barabara ya Chewoyet- tambo.
Moroto amesema kuwa hamna mahali ambapo wanakutana na gavana Lonyangapuo katika ujenzi wa barabara kwani sheria ipo wazi kuhusu barabara ambazo zinapasa kujengwa na serikali kuu na zile zinazopasa kujengwa na serikali ya kaunti.
Wakati uo huo Moroto amesema kuwa shilingi milioni 64 zimetengwa kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya kutoka chepnyal hadi Nakwijit na barabara zingine mbali mbali eneo bunge la Kapenguria ili kuhakikisha shughuli za uchukuzi zinaendelea bila tatizo.