MLINZI WA KENGEN AUGUZA MAJERAHA KWA KUVAMIWA NA WAHALIFU LOROGON.
Mkazi mmoja wa kutoka eneo la Lorogon kaunti ya Pokot magharibi anauguza majeraha katika hospitali ya kapenguria baada ya kupigwa risasi na wavamizi wanaoshukiwa kutoka kaunti jirani jumanne usiku.
Kulingana na taarifa ya idara ya polisi, Isaac Longirinyany ambaye ni mlinzi wa binafsi katika kampuni ya umeme ya KenGen, alivamiwa mwendo wa saa tatu usiku akiwa kazini kwenye zamu ya usiku na kupigwa risasi mkononi.
“Mlinzi wa binafsi wa kampuni ya KenGen alivamiwa usiku wa jumanne saa tatu na dakika kumi na kupigwa risasi mkononi na wavamizi ambao wanaaminika kutoka kaunti ya Turkana. kwa sasa yuko katika hospitali ya Kapenguria ambapo anaendelea kupokea matibabu.” Ilisema taarifa.
Hata hivyo hali yake ya afya imeendelea kuimarika huku maafisa wa usalama wakitumwa eneo hilo ili kushika doria.
“Kwa sasa hali ya mwathiriwa imeimarika. Tumetuma vikosi vyetu vya polisi eneo hilo ili kuimarisha usalama na kuendeleza msako dhidi ya wahalifu waliotekeleza uvamizi huo.”
Eneo hilo la Lorogon ni moja ya maeneo ambayo yamekuwa yakishuhudia utovu wa usalama kwa muda sasa huku oparesheni ya kuwakabili wahalifu ambao wamekuwa wakitekeleza wizi wa mifugo ikiendelea maeneo hayo ya mipakani.