MKUTANO WA AMANI BONDE LA KERIO WAANDALIWA TOT.


Viongozi kutoka kaunti tatu za kaskazini mwa bonde la ufa ikiwemo kaunti hii ya Pokot magharibi, Elgeyo marakwet na Baringo wameelezea imani kuwa juhudi za kurejesha amani eneo hili kutokana na mikakati inayowekwa zitazaa matunda.
Wakizungumza baada ya kikao cha usalama na waziri wa maswala ya ndani ya nchi Dkt Fred Matiangi eneo la Tot viongozi hao wakiongozwa na gavana wa kaunti hii John Lonyangapuo mwenzake wa Elgeyo marakwet Alex Tolgos na Stanley Kiptis wa Baringo aidha wametoa wito kwa wakazi wa maeneo haya kuchangia juhudi hizo kwa kudumisha amani.
Wakati wa kikao hicho Matiangi amesema kuwa serikali itatuma kitengo maalum cha maafisa wa usalama wa kukabiliana na uhalifu eneo hili.
Aidha ametangaza kujengwa kituo cha polisi eneo la Chesogon kuanzia juma lijalo, huku akitaka kitengo maalum kitakachotumwa eneo hilo kuwakamata wahalifu wote ambao wamekuwa wakiwahangaisha wakazi kwa muda katika kipindi cha siku saba zijazo.