MKUTANO WA AMANI BAINA YA JAMII ZA POKOT NA SEBEI WATIBUKA JAMII YA POKOT IKITAJWA KUWA KERO.
Na Benson Aswani.
Serikali ya kaunti ya Pokot magharibi kwa ushirikinao na ile ya taifa jirani la Uganda zinaendeleza mikakati ya kudumisha amani na ushirikiano miongoni mwa jamii za Pokot na Sebei ambazo zinaishi katika taifa hilo la Uganda.
Akizungumza katika mkutano eneo la Chapsukunya wilaya ya Kwen uliowaleta pamoja viongozi wa jamii ya Pokot na Sebei, naibu gavana kaunti ya Pokot magharibi Robert Komole alisema wanalenga kuwashawishi wakazi wa jamii ya Sebei kuwaruhusu wafugaji kutoka jamii ya Pokot kulisha mifugo wao eneo hilo kutokana na ukame ambao umeathiri pakubwa mifugo wao.
Komole alisema japo mazungumzo hayo hayajazaa matunda, hadi kufikia sasa ana imani kwamba suluhu itapatikana hivi karibuni.
“Tumejaribu kufanya mazungumzo na jamii ya Sebei eneo la Chepsukunya ili kupata mwafaka wa kuwaruhusu wakazi wa jamii ya Pokot kulisha mifugo wao eneo hilo. Lakini kufikia sasa hatujaafikia mwafaka wowote lakini nina imani kwamba tutaweza kupata mwafaka hivi karibuni.” Alisema Komole.
Hata hivyo viongozi waliowakilisha jamii ya Sebei waliwalaumu wakazi kutoka jamii ya Pokot kwa kile walidai kwamba kutoshirikiana nao katika juhudi za kuhakikisha amani kwa kulisha mifugo wao katika ardhi ya Sebei huku baadhi wakitoweka na mifugo wa jamii hiyo.
“Wenzetu wa jamii ya Pokot hawajaonyesha nia ya kuleta ushirikiano katika mchakato huu. Tunavyozungumza sasa tayari wanalisha mifugo wao katika ardhi yetu bila ya idhini yoyote.” Walisema.
Viongozi kutoka jamii ya Pokot wakiongozwa na mwakilishi wa kike eneo la Amudat waliomba msamaha kwa niaba ya jamii ya Pokot na kuhimiza haja ya kuwepo na ushirikiano baina ya jamii hizo ili kuafikiwa mwafaka kuhusiana na swala la lishe ya mifugo.
“Ni kweli kwamba watu wetu hawajajiendesha vyema muda huu wote, na tunaahidi kwamba tutafanya kila tuwezalo kuhakikisha kwamba wanatoa ushirikiano kwenye mchakato huu mzima wa kuleta uwiano na kuhakikisha kwamba wanapata lishe kwa ajili ya mifugo wao.” Walisema.