MKAGUZI WA BAJETI AAHIDI KUFUATILIA MIRADI AMBAYO INATEKELEZWA KATIKA KAUNTI YA POKOT MAGHARIBI.
Mdhibiti wa bajeti Margaret Nyakango yuko kaunti ya Pokot magharibi katika shughuli ya kukagua jinsi ambavyo serikali ya kaunti hiyo inaendeleza miradi mbali mbali na jinsi ambavyo fedha zimetumika katika kuitekeleza miradi hiyo.
Akizungumza baada ya kukutana na gavana Simon Kachapin afisini mwake, Nyakango alisema kwamba lengo kuu la ziara yake ni kukagua miradi, jinsi miradi hiyo imefadhiliwa na kutoa ushauri wa kifedha katika utakelezwaji wa miradi hiyo.
Nyakango tayari amekagua miradi mbali mbali hasa katika sekta ya afya, pamoja na jumba la spika ambalo ujenzi wake ulisitishwa akiahidi kufuatilia swala hilo.
“Tumekuja hapa ili kukagua miradi na kuangazia jinsi ambavyo miradi hiyo imefadhiliwa pamoja na kutoa ushauri wa kifedha kuhusu miradi inayotekelezwa. Tayari tumekagua miradi katika sekta ya afya pamoja na jumba la spika ambalo lilikwama, na ambalo tutafuatilia ili tujue mazingira yaliyosababisha kukwama jumba hilo.” Alisema Nyakango.
Gavana wa kaunti hiyo Simon Kachapin alisema ziara ya Nyakango katika kaunti hiyo ni muhimu hasa katika kutoa ushauri kuhusu maswala ya bajeti, taratibu na sheria kuhusu maswala ya kifedha ili kuwezesha serikali yake kushirikiana vyema na afisi ya mkaguzi huyo wa bajeti.
“Ziara ya mdibiti wa bajeti katika kaunti hii ni muhimu kwa sababu atatusaidia katika ushauri kuhusu maswala ya bajeti na taratibu za kisheria kuhusiana na maswala ya fedha. Hatua hii itatusaidia sisi kama kaunti kushirikiana vyema na afisi yake katika maswala mbali mbali hasa ya kifedha.” Alisema Kachapin.