MJADALA KUHUSU UAGIZAJI WA MAHINDI YA GMO WAZIDI KUTOKOTA NCHINI.

Mbunge wa Pokot kusini katika kaunti hii ya Pokot magharibi David Pkosing amemshutumu vikali waziri wa biashara, uwekezaji na viwanda Moses Kuria kufuatia kauli kwamba serikali inapanga kuagiza mahindi magunia milioni 10 yaliyokuzwa kijenetiki GMO.

Pkosing alielezea kushangazwa na kauli ya kuria akimtaka kusitisha mpango huo mara moja.

Pkosing alisema kwamba kuagizwa kwa mahindi hayo kutachangia kuzorota bei ya mahindi humu nchini hasa ikizingatiwa kwamba wakulima katika eneo la kaskazini mwa bonde la ufa na magharibi ya nchi wanaendelea kuvuna mazao yao.

“Kwa sasa wakulima maeneo ya Northrift na magharibi ya nchi wanavuna mahindi na iwapo serikali itaagiza mahindi jinsi inavyopanga basi hatua hiyo itawaathiri sana wakulima maeneo haya. Wengi wao wanategemea mahindi kuwa pato lao na iwapo mahindi ya kuagizwa yataletwa nchini huenda wakakadiria hasara.” Alisema Pkosing.

Badala yake Pkosing aliitaka serikali kununua mahindi kutoka kwa wakulima hao ili kuwasaidia waathiriwa wa baa la njaa ambalo linashuhudiwa maeneo kadhaa humu nchini kutokana na ukame ambao umekithiri maeneo hayo.

Alipendekeza mahindi ya GMO kuagizwa mwezi machi mwaka ujao wakati ambapo wakulima watakuwa wanaendeleza shughuli za upanzi.

“Badala ya kuagiza mahindi ya GMO kutoka mataifa ya nje serikali inapasa kununua mahindi kutoka kwa wakulima wa humu nchini ili kuwainua kiuchumi ikizingatiwa waligharamika zaidi katika shughuli za upanzi kufuatia kupanda bei ya pembejeo.” Alisema.