MITIHANI YA KCPE NA KPSEA YAANZA HUKU VIONGOZI MBALI MBALI WAKIWATAKIA WATAHINIWA HERI NJEMA.

Mitihani ya kitaifa kwa darasa la nane KCPE na gredi ya sita KPSEA ikiwa imeanza rasmi viongozi mbali mbali kaunti ya Pokot magharibi wameendelea kuwatakia heri njema watahiniwa wanaofanya mitihani hiyo mwaka huu.

Wa hivi punde kuwatakia wanafunzi hao heri njema ni aliyekuwa seneta wa kaunti hiyo Samwel Poghisio ambaye amewahimiza wanafunzi hao kutohofu wanapofanya mitihani hiyo bali kuwa na ujasiri kwani wameandaliwa vyema na walimu wao katika kipindi ambacho wamekuwa darasani.

Aidha Poghisio aliwahimiza watahiniwa hao kutohusika visa vya udanganyifu ambavyo huenda vikapelekea kufutiliwa mbali matokeo yao na badala yake kutumia ujuzi ambao wamepata kutoka kwa walimu wao ili wapate matokeo wanayostahiki.

“Nawakumbusha hawa watahiniwa kwamba upo tayari kwa kupita huu mtihani. Hamna haja ya kuongeza mambo ya kuiba mtihani. Umechukua miaka hiyo yote kufunzwa, sasa ni wakati wa kujipa moyo na kujiambia kwamba unaweza kufaulu.” Alisema Poghisio.

Wakati uo huo Poghisio aliwataka walimu kutowasaidia watahiniwa kushiriki wizi wa mitihani na badala yake kuwapa nafasi ya kufanya mitihani hiyo, akiwaonya pia dhidi ya matapeli ambao wanadai kuwa na makaratasi ya mitihani hiyo.

“Hao walimu ambao wanawahadaa wanafunzi kwamba watawasaidia kuiba mtihani, aibu kwao. Nyinyi ni walimu ambao mmepokea mafunzo ya kuwaandaa wanafunzi. Wape nafasi wakati wa mitihani kufanya kile wanachoelewa ili wapate matokeo ambayo wanastahiki.” Alisema.