MIRADI YA MAENDELEO POKOT MAGHARIBI YATARAJIWA KUKAMILIKA KABLA YA AGOSTI 9.


Serikali ya kitaifa iko mbioni kukamilisha miradi iliyoanzishwa katika kaunti mbali mbali nchini kabla ya kukamilika muhula wa pili wa kuhudumu rais Uhuru Kenyatta ambaye anatarajiwa kustaafu tarehe 9 mwezi agosti mwaka huu.
Akizungumza mjini Kapenguria kaunti hii ya Pokot magharibi, katibu katika wizara ya huduma za umma, jinsia na mipango maalum kitengo cha maeneo kame Mikah Powon amesema kuwa ipo baadhi ya miradi ambayo tayari imekamilika katika kaunti hii huku miradi mingine ikiwa katika awamu za mwisho mwisho kabla ya kukabidhiwa serikali ya kaunti.
Miongoni mwa miradi hiyo ni pamoja kichinjio cha Nasukuta na kiwanda cha maziwa eneo la Lelan pamoja na mradi wa maji wa Siyoi Muruny.
Hata hivyo Powon amesema kuwa miradi ambayo haitakuwa imekamilika kufikia mwezi agosti wakati rais Kenyatta atakapostaafu itakabidhiwa serikali itakayochukua hatamu ya uongozi ili kuendelezwa na kukamilishwa.