MIMBA ZA MAPEMA ZASALIA KIKWAZO KWA ELIMU YA MTOTO WA KIKE POKOT MAGHARIBI.


Huenda baadhi ya wanafunzi hasa wa kike katika kaunti hii ya Pokot magharibi wakakosa kurejea shuleni baada ya shule kufunguliwa tena kutokana na likizo ya majuma mawili ambayo yalitumika kuandaa uchaguzi mkuu mchini.
Kulingana na naibu mwalimu mkuu wa shule ya upili ya wasichana ya Nasokol Dina Mnang’at hadi kufikia sasa asilimia 15 ya wanafunzi hawajarejea shuleni akielezea hofu huenda baadhi yao wamelazimika kusitisha masomo kutokana na baadhi ya jamii katika kaunti hii kuendelea kushikilia tamaduni zilizopitwa na wakati.
“Takriban asilimia 85 ya wanafunzi wamerejea shuleni na huenda asilimia 15 hawataweza kurejea labda kufuatia maswala ya kitamaduni ambapo baadhi ya wazazi wanaona ni heri wamwoze mtoto wa kike wapate mahari kuliko kumpeleka shule.” Alisema.
Mnang’at alisema kuwa swala la mimba za mapema miongoni mwa wanafunzi lingali changamoto katika kaunti hii ya Pokot magharibi baadhi ya wanafunzi wakilazimika kusitisha masomo yao kutokana na hali hii japo wako wale ambao wanaendelea na masomo wakiwa wajawazito.
“Mimba za mapema bado ni changamoto ambapo uchunguzi wetu mapema mwaka huu ulibaini kuwa bado ipo asilimia moja ya wanafunzi ambao walikuwa wajawazito. Wapo baadhi ambao waliacha masomo, ila wapo ambao wanaendelea na masomo.” Alisema.
Alielezea umuhimu wa kuendelezwa uhamasisho miongozi mwa wanajamii hasa maeneo ya mashinani ambako anasema kuwa elimu haithaminiwi ili kuwafahamisha wazazi kuhusu umuhimu wa kumwelimisha mtoto wa kike.
“Wadau wote wanafaa kuchukua hatua ya kuwahamasisha wananchi hasa maeneo ya mashinani wasiothamini elimu ya mtoto wa kike ili wafahamu umuhimu wa kumwelimisha mtoto wa kike.” Alisema Mnang’at.