MIMBA ZA MAPEMA ZASALIA KERO POKOT MAGHARIBI.


Takwimu za shirika la AMREF zinaashiria kuwa visa vya mimba za mapema katika kaunti hii ya Pokot magharibi zinazidi viwango vya kitaifa.
Haya ni kwa mujibu wa mshirikishi wa shirika hilo John Ambiut ambaye amesema kuwa huenda hali ni mbaya zaidi kuliko inavyodhaniwa na kuongeza kuwa ili kukomesha visa hivi italazimu kuwepo ushirikiano wa wadau kutoka katika sekta mbali mbali ikiwemo za serikali ya kitaifa pamoja na ya kaunti.
Amesema kuwa ni wakati sheria zinazohusu kurejea shuleni kwa wanafunzi waliopachikwa mimba kuangaliwa upya kutokana na hali kuwa zipo baadhi ya shule zinazowafukuza wanafunzi waliopachikwa mimba, huku pia akitaka jamii kuweka mikakati ya jinsi ya kukabili mimba za mapema.
Kwa upande wake spika wa bunge la kaunti hii ya pokot magharibi Christine Apakoreng amesema kuwa kumebuniwa kundi la wadau kutoka sekta mbali mbali za serikali pamoja na mashirika yasiyo ya serikali litakalohakikisha visa hivi vinakabiliwa, akiongeza kuwa serikali ya kaunti imejitolea kikamilifu katika juhudi hizo.
Kulingana na msimamizi wa maswala ya utamaduni katika jamii ya pokot William Lopetakou visa vya mimba za mapema vimeongezeka katika kaunti hii kutokana na hali kuwa jamii imekiuka tamaduni ambazo zilisaidia pakubwa kukabili visa hivi.