MIMBA ZA MAPEMA NA TATIZO LA KARO YATAJWA MIONGONI MWA SABABU ZA KUTOFANYA VYEMA KATIKA KCSE BAADHI YA WANAFUNZI.


Visa vya mimba za mapema miongoni mwa baadhi ya wanafunzi wa kike kaunti ya Pokot magharibi pamoja na tatizo la karo ni baadhi ya changamoto ambazo zilipelekea baadhi ya shule kutofanya vyema jinsi ilivyotarajiwa katika mtihani wa kitaifa wa KCSE mwaka 2022.
Kulingana na mwalimu mkuu wa shule ya upili ya wasichana ya St Bakhita Grace Kakuko, licha ya juhudi za wadau mbali mbali na mikakati kadhaa iliyowekwa kukabili visa vya mimba za mapema miongoni mwa wanafunzi, tatizo hili limesalia changamoto kwa elimu ya mtoto wa kike.
Wakati uo huo Kakuko alisema wengi wa wanafunzi ambao wangefanya vyema katika mtihani huo walitatizika pakubwa kutokana na tatizo la karo ambapo baadhi walikosa kabisa kufanya mtihani huo huku baadhi walionafasika kuufanya wakikosa kufanya vyema kufuatia kipindi kirefu ambacho walikosa kuhudhuria masomo shuleni.
“Wanafunzi wetu wengi ambao wangefanya vyema katika mtihani wa KCSE walikabiliwa na changamoto mbali mbali. Mfano kuna wale ambao walipata mimba na wakaishia kuacha masomo. Wengine walikumbwa na tatizo la karo ambapo hawakuwa shuleni kwa kipindi kirefu hali hii ikachangia kutofanya vyema katika mtihani huo.” Alisema Kakuko.
Kauli yake kakuko inajiri wakati ambapo kamati ya elimu katika bunge la kitaifa inatarajiwa kuanzisha uchunguzi kuhusiana na matokeo hayo ya mwaka 2022 kufuatia madai kwamba huenda kulikumbwa na udanganyifu mkubwa katika mtihani huo kufuatia idadi kubwa ya watahiniwa waliopata alama ya A.