MIMBA NA NDOA ZA MAPEMA ZASALIA CHANGAMOTO SIGOR.


Swala la mimba pamoja na ndoa za mapema miongoni mwa wanafunzi limeendelea kuwa changamoto kwa elimu ya mtoto wa kike katika shule za eneo la sigor Pokot ya kati katika kaunti hii ya Pokot magharibi.
Wakiongozwa na mkuu wa shule ya Upili ya wasichana ya ELCK Chesta eneo la Sigor Patricia Nandi, wakuu wa shule eneo hilo wamesema kuwa idadi ya wanafunzi wa kike ambao wanajiunga na vyuo vikuu kutoka eneo hilo ni ya chini mno kutokana na tatizo hilo la mimba na ndoa za mapema.
Nandi amesema uchunguzi wao umebaini kuwa umasikini miongoni mwa wazazi wengi pamoja na mapuuza kuhusu umuhimu wa elimu kwa wanao ni miongoni mwa maswala makuu ambayo yanachangia pakubwa kukithiri visa hivi eneo hilo.
Ametoa wito kwa wazazi kuzingatia umuhimu wa elimu ya wanao na kutowaoza mapema na badala yake kuwapa muda walimu kuwafunza, huku pia akitaka swala la kupachikwa mimba wanafunzi kutosuluhishwa nyumbani, ila sheria kuchukua mkondo wake kwa wanaopatikana na hatia hiyo.