MIKWARUZANO YA KISIASA YAENDELEA TRANS NZOIA KUFUATIA SHINIKIZO LA KUBUNIWA KAUNTI MPYA YA MLIMA ELGON.

Viongozi wa chama cha Ford Kenya katika kaunti ya Trans nzoia wamewakosoa vikali baadhi ya viongozi katika kaunti hiyo ambao wanashinikiza kubuniwa kaunti mpya ya mlima Elgon kwa kumlaumu gavana wa kaunti hiyo George Natembeya ambaye wamemtaja kuwa kizingiti kwa juhudi hizo.

Wakiongozwa na Benson Simiyu, viongozi hao walisema japo Natembeya alichaguliwa kupitia chama tofauti na Ford Kenya, chama hicho kimeridhishwa na utendakazi wake na kamwe hakitaruhusu viongozi ambao wanashinikiza maslahi yao ya kibinafsi kumharibia sifa.

Simiyu alisema kwamba gavana Natembeya alizingatia usawa katika uteuzi wa maafisa wanaohudumu kwenye serikali yake, na kwamba jamii zote ambazo zinaishi katika kaunti hiyo zimewakilishwa vilivyo katika serikali yake.

“Nawaambia hawa viongozi kwamba hatutaki migawanyiko ya kikabila kaunti hii. Sisi ni wanachama wa Ford Kenya lakini tulianguka kura. Gavana aliyepo sasa ni Natembeya na tumeridhishwa na kazi ambayo anafanya. Serikali yake imezingatia usawa katika jamii zote zinazopatikana kaunti hii.” Alisema Simiyu.

Baadhi ya viongozi kutoka jamii ya Sabaot wakiongozwa na aliyekuwa mwakilishi wadi ya Saboti David Kapoloman na Lawrence Mogusu ambaye alikuwa mwakilishi wadi ya Kinyoro, wamekuwa msitari wa mbele kushinikiza kubuniwa kaunti mpya ya mlima Elgon, huku wakimlaumu gavana Natembeya kwa kile wamedai amekuwa kizingiti kwa mchakato huo.

“Tumenyanyaswa miaka mingi katika uongozi wa kaunti hii ya Trans nzoia. Sisi kama jamii hatujawakilishwa inavyofaa tangu kuanza kutekelezwa serikali za ugatuzi hapa nchini. Na sasa tunachotaka ni kaunti yetu. Hata kama gavana Natembeya anajaribu kuwa kikwazo tutang’ang’ana hadi tupate kaunti yetu.” Walisema.