‘MIKAKATI ZAIDI YAHITAJIKA KUWAREJESHA WATOTO SHULENI’, YASEMA KNEC

Na Benson Aswani
Siku moja baada ya idara ya usalama kwa ushirikiano na wadau wengine kaunti hii ya Pokot magharibi kutangaza kuanza oparesheni ya kuhakikisha watoto wote katika kaunti hii wanarejeshwa shuleni wito umetolewa wa kuwekwa mikakati zaidi ili kuhakikisha kuwa juhudi hizo zinafanikishwa.
Mwenyekiti wa baraza la mitihani nchini KNEC tawi la Pokot magharibi Aineah Simiyu amesema kuwa kampeni ya kuwahamasisha wakazi kuhusu swala hilo inapasa kuanzishwa ikiwemo kuchapisha jumbe za kuwarejesha watoto shuleni kwenye mavazi ili kupiga jeki juhudi hizo.
Aidha Simiyu amesema kuwa oparesheni kama hizo mara nyingi hukumbwa na changamoto tele ikiwemo ukosefu wa ushirikiano kutoka kwa baadhi ya wazazi akisema kuwa mikakati zaidi inapasa kuwekwa katika kuwatafuta watoto hao hasa maeneo ya mashinani.