MIKAKATI YAENDELEZWA KUDUMISHA AMANI BAINA YA JAMII ZA POKOT, SEBEI NA KARAMOJONG, UGANDA.

Hali ya utulivu inaendelea kushuhudiwa baina ya jamii za pokot, sebei na karamojong zinazoishi katika taifa jirani la Uganda, kufuatia mikakati ya amani ambayo inaendelea kuwekwa na uongozi wa taifa hilo kwa ushirikiano na kaunti ya Pokot magharibi.

Mwakilishi wa jamii ya Pokot katika bunge la Uganda Mika Alolem alisema kwamba kwa sasa wanaendeleza mikutano ya amani baina ya jamii hizo ili kupata suluhu ya kudumu kwa tatizo hilo la wizi wa mifugo.

Aidha Alolem alisema kwamba shughuli ya kuondoa silaha zinazomilikiwa kinyume cha sheria na wakazi inaendelea kama njia moja ya kuhakikisha usalama unadumishwa.

“Kwa sasa hali maeneo haya imetulia na tunaendeleza mikutano ya amani baina ya jamii hizi, pamoja na kuhakikisha kwamba silaha zinazomilikiwa kinyume cha sheria zinaondolewa ili kuwe na amani ya kudumu.” Alisema Alolem.

Wakati uo huo Alolema alipongeza ushirikiano baina ya kaunti ya Pokot magharibi na taifa la Uganda ambao umesaidia kurejeshwa kwenye taifa hilo mifugo wa jamii ya Sebei walioibwa na watu waliokisiwa kutoka kaunti ya Pokot magharibi.

“Nashukuru sana serikali ya Pokot magharibi kupitia maafisa wa serikali eneo la Kacheliba kwa kushirikiana na serikali ya Uganda na kuhakikisha kwamba mifugo walioibwa na watu kutoka upande wa pokot wanarejeshwa.” Alisema.