MIKAKATI YA KUANDAA CHAGUZI ZILIZOAHIRISHWA YAKAMILIKA.
Baadhi ya wagombea nyadhifa za uongozi katika maeneo ambako uchaguzi mkuu uliahirishwa wameelezea kuridhia tarehe mpya ya uchaguzi huo iliyotangazwa na tume ya uchaguzi IEBC.
Mwenyekiti wafula chebukati alisema tume hiyo imewapa wagombea hao siku nne za kufanya kampeini na kusitishwa siku ya ijumaa masaa 48 kabla ya kuandaliwa uchaguzi huo siku ya jumatatu.
Mbunge wa pokot kusini kaunti hii ya Pokot Magharibi ambaye pia analenga kutetea kiti hicho kupitia tiketi ya chama cha KUP David Pkosing amesema amekubaliana na tarehe hiyo huku akitaka tume hiyo kuhakikisha vifaa vya kiems vinafanya kazi ili kuhakikisha kila mtu atapiga kura jumatatu ijayo bila matatizo.
“Nakubaliana na tarehe hiyo mpya ya tume ya uchaguzi ila nataka niiambie tume hiyo iweke mikakati ya kuhakikisha kwamba hakuna mpiga kura atakayekosa kupiga kura kutokana na mitambo ya Kiems kukosa kusoma alama za vidole.” Alisema.
Aliongeza kuwa,”kutokana na makali ya jua maeneo haya, watu wetu wengi wameathiriwa na alama zao za vidole hazionekani. Ni kutokana na hali hii ambapo baadhi ya wapiga kura hawakupiga kura katika uchaguzi mkuu wa agosti 9.”
Naye mgombeaji kiti hicho kwa tiketi ya chama cha UDA simon kalekem aliitaka tume ya uchaguzi IEBC kuwatuma maafisa wapya ambao watasimamia uchaguzi maeneo hayo kando na waliotekeleza jukumu hilo agosti 9.
“Tunahitaji kuwa na maafisa wapya wa kusimamia chaguzi za pokot kusini na Kacheliba ili kwamba tukaweze kuwa na uchaguzi ambao ni huru.” Alisema.
Alisema baada ya kikao hicho anatumai uchaguzi huo utakuwa huru na wa haki.