MIITO YA SIASA ZA AMANI YAENDELEA KUTOLEWA NA VIONGOZI WA KIDINI.

Na Benson Aswani
Viongozi wa kidini katika kaunti hii ya Pokot magharibi wametoa wito kwa wanasiasa nchini kuendeleza siasa za amani wakati huu ambapo taifa linajiandaa kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa mwaka ujao.
Wakiongozwa na mchungaji wa kanisa la Redeemed mjini Makutano kaunti hii ya Pokot magharibi Rev. Robert Nato, viongozi hao wametoa wito kwa wadau ikiwemo idara za usalama pamoja na makanisa kuhimiza utangamano nchini ili kuzuia hali zilizoshuhudiwa katika chaguzi zilizotangulia nchini.
Aidha Nato amewataka viongozi wa kisiasa katika kaunti hii ya pokot magharibi kuendesha siasa komavu za kuuza sera zao na kukoma kushambuliana katika majukwaa ya kisiasa kwani ni mpiga kura ndiye atakayeamua kiongozi atakayemchagua katika uchaguzi mkuu ujao.
Wakati uo huo Nato ameziomba idara za usalama kaunti hii kuimarisha usalama katika maeneo ya mipaka ya kaunti hii na taifa jirani la Uganda, kufuatia shambulizi la kigaidi lililoshuhudiwa nchini humo ambapo watu watatu waliaga dunia huku wengine wengi wakijeruhiwa.