MIITO YA MSAADA WA CHAKULA POKOT MAGHARIBI YAENDELEA, IDADI YA WAATHIRIWA WA BAA LA NJAA IKIZIDI KUONGEZEKA.
Wahisani mbali mbali na mashirika ya kijamii yametakiwa kujitokeza na kuwasaidia wakazi wa maeneo mbali mbali ya kaunti hii ya Pokot magharibi ambao wanakabiliwa na baa la njaa kufuatia ukame unaoshuhudiwa nchini.
Ni wito wake naibu spika wa bunge la kaunti ya Pokot magharibi Victor Siywat ambaye alisema kwamba idadi kubwa ya wakazi wa kaunti hiyo wanakabiliwa na baa la njaa na itakuwa bora iwapo watashughulikiwa jinsi inavyofanyika katika maeneo mengine ya nchi.
Wakati uo huo Siywat alisema mipango inaendelea miongoni mwa manaibu spika nchini kupitia muungano wao kuchangisha fedha zitakazosaidia kuwasaidia waathiriwa na baa la njaa kaunti ya Pokot magharibi na maeneo mengine ya nchi.
“Maeneo mengi ya kaunti hii yanakabiliwa na baa la njaa. Wakazi wengi wanaumia kwa sababu ya njaa. Tunatoa wito kwa mashirika kijamii waje watusaidie. Kwa sasa tuna kikundi chetu cha manaibu spika Kenya nzima na tunajipanga kuchanga fedha kidogo kuwasaidia waathiriwa.” Alisema Siywat.
Ni wito ambao ulisisitizwa na katibu wa kaunti hiyo Jonathan Siwanyang ambaye aidha aliitaka serikali kuu kutoa fedha ambazo zilipitishwa na bunge la kitaifa za kununua chakula kwa ajili ya waathiriwa wa baa la njaa.
“Nataka niisihi serikali kuu kuharakisha kutoa fedha ambazo zilipitishwa na wabunge hivi majuzi kusaidia katika kukabili baa la njaa katika kaunti hii yetu ya Pokot magharibi.” Alisema Siwanyang.