MIITO YA MISAADA YATOLEWA HUKU BAA LA NJAA LIKIENDELEA KUKITA MIZIZI TURKANA.
Mwenyekiti wa jamii ya Turkana kaunti ya Trans nzoia Jackson Eragai amewataka wanasiasa, wafanyibiashara na watu wenye nia njema kutoa msaada wa chakula kwa wakazi wa kaunti ya Turkana ili kuokoa maisha ya waathiriwa.
Akizungumza na wanahabari mjini Kitale Eragai aidha ameitaka serikali kuu kuhakikisha kwamba misaada ambayo inatolewa na wahisani mbali mbali inawafikia waathiriwa halisi.
“Marafiki wetu wa Trans nzoia ambao ni matajiri wa mahindi, viongozi wetu wa kisiasa na wenye nia njema ambao wanaweza kusaidia wananchi, tafadhali mjaribu kuchanga chochote msaidie watu wetu ambao wanaathirika na baa la njaa kaunti ya Turkana.” Alisema Eregai.
Eregai aliendelea kusema, “Natoa wito kwa serikali kwamba chakula kikishatolewa, tafadhali mhakikishe kwamba kinawafikia watu wanaokusudiwa ili isiwe tena ni biashara kwa manufaa ya kibinafsi ya watu wachache.”
Ni kauli ambayo ilitiliwa mkazo na aliyewania useneta katika kaunti hiyo ya Trans nzoia na ambaye pia ni kiongozi wa makundi mbali mbali ya akina mama kaunti hiyo Beatrice Kitiabi.
“Hili swala la njaa katika kaunti ya Turkana linanikera sana. Ukiona watoto wakihangaika kwa sababu ya njaa na sisi tuna chakula inaniudhi sana. Kwa hivyo natoa wito kwa kina mama wa trans nzioa wakiongozwa na naibu gavana tuonyesha mfano mwema kwa kuchangisha chakula kwa ajili ya wenzetu huko Lodwar.” Alisema Kitiabi.