MIITO YA KUREJESHWA KIBOKO SHULENI YAENDELEA KUTOLEWA.

Na Benson Aswani
Viongozi katika kaunti ya Baringo sasa wanapendekeza kurejeshwa kwa adhabu ya viboko shuleni ili kukabili utovu wa nidhamu miongoni mwa wanafunzi ambao unatajwa kuwa moja ya sababu ya kuendelea kuripotiwa mikasa ya moto shuleni.
Wakiongozwa na naibu gavana Jacob Chepkwony viongozi hao wamesema kuwa wanafunzi wengi wamekuwa watukutu na kukosa nidhamu tangu serikali ilipoharamisha adhabu ya viboko.
Chapkwony aidha amesema kuwa huenda visa vya kuteketezwa mabweni vimechangiwa na shinikizo za kimasomo ambazo zimesababishwa na mabadiliko katika kalenda ya masomo ambayo iliathiriwa na janga la korona.
Kwa upande wake spika wa bunge la kaunti ya Baringo David Kerich amewataka walimu wakuu kufuatilia kwa karibu mienendo ya wanafunzi wao na vile vile wazazi kila wakati wanao wanapokuwa nyumbani.
Naye mwaniaji wa wadhifa wa uwakilishi akina mama Susan Chesina amevitaka vyombo vya habari kutoipa kipau mbele matukio ya mikasa ya moto shuleni akisema kuwa huenda hali hiyo inachangia kuendelea kuripotiwa kwa visa hivyo.