MIITO YA KUDUMISHWA AMANI YAZIDI KUTOLEWA SIKU 4 TU KABLA YA UCHAGUZI MKUU.


Siku nne tu kabla ya uchaguzi mkuu wa jumanne juma lijalo mwaniaji ugavana katika kaunti hii ya Pokot magharibi kupitia chama cha UDA Simon Kachapin ametoa wito kwa wakazi wa kaunti hii kujiandaa kujitokeza kwa wingi kushiriki zoezi hilo muhimu.
Kachapin ambaye ni gavana wa kwanza wa kaunti ya Pokot magharibi aidha ametoa wito kwa wakazi kuendelea kudumisha amani kipindi hiki cha uchaguzi na kuwapa nafasi wagombea wote kuuza sera zao katika kipindi cha lala salama kabla ya kukamilika rasmi kipindi cha kampeni.
Wakati uo huo Kachapin amewataka wanasiasa wote wanaotafuta nyadhifa za uongozi kutumia kipindi hiki kilichosalia kuhubiri amani miongoni mwa wakazi.
“Nataka kuwahimiza watu wote wajitokeze kwa wingi tarehe 9 wakuje wapige kura kwa wingi. Pili ningewaomba wakazi wa west pokot na hata majirani zetu na Kenya kwa ujumla, kwamba wakati huu tuhubiri amani, tufanye siasa ya amani, tusikilize kila mmoja.” Amesema Kachapin.
Ni kauli ambayo imesisitizwa na seneta wa kaunti hiyo Samwel Poghisio ambaye analenga kuhifadhi kiti hicho katika uchaguzi mkuu ujao ambaye aidha amezitaka kamati zinazoshughulika na amani kuzuru maeneo yote ya kaunti hii na kaunti jirani katika juhudi za kuhakikisha kuwa kunashuhudiwa amani katika uchaguzi wa juma lijalo.
“Katika mipaka yetu ya Pokot/Turkana, Pokot/Uganda, Pokot/Marakwet, upande wa sebei na upande wa Trans nzoia tuwe na amani wakati huu wa uchaguzi. Kamati za amani mfanye kazi yenu, muanze kutembea kuhakikisha kwamba tuna amani katika uchaguzi huu.” Amesema Poghisio.
Miito ya wawili hao imejiri wakati ambapo kumekuwepo madai ya kusambazwa vijikaratasi vya kueneza chuki katika baadhi ya kaunti za bonde la ufa ikiwemo kaunti ya Baringo na ile ya Uasin Gishu.
Siku chache zilizopita waziri wa maswala ya ndani ya nchi Dkt. Fred Matiangi alithibitisha kukamatwa washukiwa 8 wanaouhusishwa na kusambazwa vijikaratasi hivyo vinavyolenga jamii moja katika kaunti hizo.