MIITO YA AMANI YAENDELEA KUTOLEWA TAIFA LIKIELEKEA KWENYE UCHAGUZI MKUU.
Wito umetolewa kwa wakazi wa kaunti hii ya Pokot magharibi kudumisha amani na kutokubali kutumika vibaya na wanasiasa kuvuruga amani kwa manufaa yao ya binafsi hasa wakati huu ambapo taifa linakaribia uchaguzi mkuu wa tarehe 9 mwezi agosti.
Seneta wa kaunti hii Samwel Poghisio aidha amewataka wakazi kuwa makini na kuwapiga msasa wagombea wa nyadhifa za kisiasa ili kuwachagua viongozi wenye maadili na wenye rekodi bora ya maendeleo na kutojutia baadaye maamuzi yao.
Aidha Poghisio amewataka wanasiasa kaunti hii kuendesha kampeni zao kwa njia inayokubalika kisheria na kutowatumia vijana kwa malengo yao ya kibinafsi, huku akitishia kuwataja wazi wanasiasa anaodai kuwa wanawatumia vijana kuvuruga Amani iwapo wataendelea na tabia hiyo.
Wakati uo huo Poghisio ametumia fursa hiyo kuonya dhidi ya kutumika msaada wa chakula ambao serikali kuu inatoa kwa ajili ya wakazi wa kaunti hii wanaokabiliwa na makali ya njaa kutafuta kura kutoka kwa wakazi.