MIGAWANYIKO YAENDELEA KATIKA CHAMA CHA ODM TRANS NZOIA.


Baadhi ya viongozi na wagombea wa viti mbali mbali kupitia chama cha ODM katika kaunti ya Trans nzoia wamemkashifu mbunge wa Saboti Caleb Amisi kwa kufeli kufanya kikao nao na kinara wa chama hicho Raila Odinga siku chache tu baada yake kuzuru kaunti hiyo.
Wakiongozwa na Eric Simatwa, viongozi hao wamesema ziara hiyo imezua migawanyiko kwenye chama cha ODM kutokana na hatua ya Amisi ambaye pia ni mwenyekiti wa chama kaunti hiyo ya Trans nzoia kuwatenga na kumwomba naibu wa chama gavana wa Kakamega Wyclife Oparanya kuingilia kati kuzuia mzozo zaidi chamani.
Ikumbukwe awali katibu mkuu wa chama hicho Edwin Sifuna aliagiza kufungwa akaunti zote za chama cha ODM tawi la kaunti hiyo kufuatia mzozo wa uongozi ambao umedumu kwa miezi kadhaa sasa.