MIFUGO WALIOIBWA BARINGO WAREJESHWA

NA BENSON ASWANI
Maafisa wa usalama kwa ushirikiano na wakazi wa eneo la kinyach kwenye eneo bunge la baringo kaskazini kaunti ya Baringo wamefanikiwa kuwarejesha takriban ng’ombe 40 waliokuwa wameibiwa na wavamizi wanaodaiwa kutoka kaunti jirani elgeiyo marakwet.
Wavamizi hao walilivamia eneo hilo katika shambulizi linalokisiwa kuwa la kulipiza kisasi baada ya wezi wa mifugo wanaodaiwa kutokea eneo bunge la tiaty kufanya shambulizi katika eneo bunge la marakwet mashariki mapema jumamosi.
Visa hivyo vya mashambulizi vinajiri wakati ambapo viongozi kaunti ya baringo wanaitaka serikali kuchukua hatua na kuwakabili wezi wa mifugo ambao wanaendeleza kutekeleza mashambulizi eneo bunge la baringo kaskazini na kusini.
Wakiongea katika eneo bunge la baringo kusini kufuatia kisa cha kuuliwa mtu mmoja na nyumba kadhaa kuteketezwa kwenye kijiji cha lamaiwe kwenye wadi ya mochongoi, viongozi hao wamesema kwamba serikali inastahili kufanya kila iwezalo ili kuwakabili wahalifu hao.
Naye gavana wa kaunti hiyo stanley kiptis ameitaka serikali kuu kusaidia katika kuwajenga makazi mapya wakazi ambao nyumba zao ziliteketezwa na vile vile kuwasambazia chakula cha msaada.