MHUDUMU WA BODABODA AENEZA UJUMBE WA AMANI BARINGO.
Baada ya kaunti ya baringo kuorodheshwa miongoni mwa kaunti 10 zenye uwezekano mkubwa wa kushuhudia ghasia za baada ya uchaguzi, mhudumu mmoja wa bodaboda katika kaunti hiyo amechukua jukumu la kuzuru maeneo tofauti kuwarai wakazi kudumisha amani kabla na hata baada ya uchaguzi ujao.
Mhudumu huyo kwa jina gabriel nyongesa mwenye umri wa miaka 27 mkazi wa mji wa kabarnet na ambaye pia ni msanii wa nyimbo za injili, ametundika spika, na mtambo wa jenerata kwenye pikipiki yake na kisha kuzuru miji tofauti ya kaunti hiyo kuhubiri amani kwa wakazi.
Nyongesa amesema kuwa yeye hurauka alfajiri ya kuendeleza shughuli zake za bodaboda kwa ajili ya kusaka fedha za kukidhi mahitaji ya familia yake hadi mwendo wa alasiri kisha hukodi mtambo wa jenereta na kisha kuzuru vituo vya magari, na soko kuhimiza amani miongoni mwa wenyeji.
Kulingana na nyongesa tayari amezuru miji yote mikuu ya baringo na pia baadhi ya maeneo katika kaunti ya elgeiyo marakwet katika muda wa mwezi mmoja sasa licha ya kupitia changamoto nyingi na hasaa kukosa mafuta ya petrol.
Nyongesa anasema kuwa aliafikia uamuzi wa kuchukua jukumu la kuhimiza haja wakazi kukumbatia amani na kuishi kwa umoja baada ya nduguye kupokea kifo wakati wa machafuko ya baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2007.