MGOMBEA UWAKILISHI WA LWANDANYI APUUZA MADAI YA KUJIONDOA KINYANG’ANYIRONI.

Mgombea kiti cha mwakilishi wadi ya Lwandanyi katika kaunti ya Bungoma Levy Nabangi amepuuzilia mbali uvumi ambao unaenezwa na baadhi ya wanasiasa eneo hilo kuwa amejiondoa katika kinyang’anyiro hicho na kumuunga mkono mmoja wa wapinzani wake.
Nabangi ambaye anawania kiti hicho kupitia chama cha UDA amesema kuwa hajashiriki mazungumzo yoyote kuhusu swala la kujiondoa kwenye kinyang’anyiro hicho huku akiwahakikishia wafuasi wake kwamba atakuwa debeni agosti 9.
Wakati uo huo Nabangi amewahimiza wakazi wa eneo hilo kuwapiga msasa viongozi wanaowania nyadhifa za uongozi ili kuwachagua viongozi waadilifu na watakaohakikisha maendeleo kwa wananchi.
Aidha amewashauri vijana kujitenga na wanasiasa wanaolenga kuwatumia kuzua vurugu katika mikutano ya wapinzani wao kwa manufaa yao ya binafsi na badala yake kujihusisha na maswala ambayo yatawanufaisha kimaisha.