MCHAKATO WA KUPATA UONGOZI MPYA POKOT MAGHARIBI WAELEKEA KUKAMILIKA.


Mipango ya kuingia afisini rasmi serikali mpya inayoongozwa na gavana mteule Simon Kachapin katika kaunti hii ya Pokot magharibi inaendelea, kamati ya kufanikisha ukabidhianaji mamlaka ikiwa katika hatua za mwisho kufanikisha mchakato huo.
Ikiongozwa na katibu wa kaunti John Karamunya, kamati hiyo ya wanachama 13 imetambua uwanja wa maonyesho ya kilimo wa kishaunet kuwa sehemu ambako hafla hiyo ya alhamisi tarehe 25 mwezi huu wa agosti itaandaliwa.
Karamunya amesema kuwa kamati hiyo inaweka mikakati yote ya kuhakikisha mchakato mzima wa ukabidhianaji mamlaka unaetekelezwa kwa njia inayostahili.
Kulingana na sheria magavana wateule wanapasa kuapishwa alhamisi ya kwanza baada ya siku kumi tangu kutangazwa matokeo ya mwisho ya uchaguzi na tume huru ya uchaguzi na mipaka IEBC.
Wanachama wa kamti hiyo wanajumuisha mwakilishi wa kamishina wa kaunti, mwakilishi wa huduma za polisi, mwakilishi wa idara ya ujajusi, maafisa wakuu kutoka wizara za fedha na mipango, teknolojia, utalii na tamaduni, mwakilishi kutoka bunge la kaunti na waakilishi wawili waliochaguliwa na gavana mteule.