MBUNGE WA POKOT KUSINI AKASHIFIWA KWA KULEMAZA MIRADI YA MAENDELEO ENEO HILO.


Aliyekuwa kiongozi wa wengi katika bunge la kaunti hii ya pokot magharibi kwenye serikali iliyotangulia Simon Kalekem amemshutumu mbunge wa pokot kusini David Pkosing kwa kile amedai utepetevu katika utendakazi wake.
Kalekem ambaye ametangaza nia ya kugombea kiti cha ubunge eneo hilo la Pokot kusini kupitia chama cha UDA kinachohusishwa na naibu rais William Ruto, amesema kuwa maeneo mengi ya kaunti hii ya pokot magharibi yana vyuo vya kiufundi, chuo ambacho hakipo eneo bunge hilo la pokot kusini.
Amesema kwa chuo cha kipekee ambacho kilikuwa kinajengwa eneo la Nasukuta kiliporomoka na mamilioni ya fedha kupotea na hamna hatua yoyote iliyochukuliwa kufuatia hali hiyo, huku akimtaka Pkosing kuelezea kilichojiri.
Aidha Kalekem amemsuta Pkosing kwa kulemaza mradi wa maji wa puson licha ya fedha nyingi kutumika kutekeleza mradi huo ili kuwanufaisha wakazi wa eneo hilo ila sasa wanahangaika kwa kukosa bidhaa hiyo muhimu.
Wakati uo huo amemsuta mbunge huyo kwa kutumia nafasi yake ya mwenyekiti wa kamati ya barabara katika bunge la kitaifa kuwahadaa wakazi wa eneo hilo kuwa ndiye ameshawishi ujenzi wa barabara nyingi kaunti hii ya pokot magharibi akisema barabara zote kaunti hii zimejengwa na serikali kuu.