MBUNGE WA KAPENGURIA SAMUEL MOROTO AMEWATAKA WAKAAZI WA ENEO LA KABOTO CHEPCHOINA KUISHI KWA AMANI

POKOT MAGHARIBI


Saa chache tu baada ya Kalya Radio kuangazia kisa cha baba ya watoto tisa aliyenuia kununua shamba kushambuliwa na kundi la vijana kwenye eneo la Kaboto Chepchoina, Mbunge wa Kapenguria Samuel Moroto amejitokeza na kukashifu vikali kisa hicho.
Kulingana na Moroto ni kwamba migogoro ya mashamba inayoshuhudiwa katika eneo la Chepchoina mpakani pa Pokot na kaunti ya Trans-Nzoia imehusishwa na uchochezi unaoenezwa na maafisa wa usalama katika eneo hilo.
Akizungumza baada ya kuripotiwa kwa mauaji ya jamaa mmoja katika eneo la Chepchoina, Moroto amesema wizara ya ardhi imeshindwa kutatua mvutano huo huku maafisa wa polisi wakiendelea kuwahangaisha wakazi na kutumia nguvu kupita kiasi katika harakati ya kutatua kesi za mashamba katika eneo hilo.
Moroto aidha amewataka wakazi wa eneo hilo kukumbatia umoja miongoni mwao bila kuwategemea zaidi maafisa wa polisi ikizingatiwa kwamba maafikiano ya kuleta amani miongoni mwa jamii nyingi yamefanyika kwa kuwashirikisha watu wa jamii zinazozozana wenyewe kwa wenyewe.