MAWAZIRI WAPIGWA MSASA NA BUNGE POKOT MAGHARIBI
Mawaziri waliopendekezwa kuhudumu katika baraza la mawaziri la kaunti hii ya Pokot magharibi hatimaye wamepigwa msasa na kamati ya bunge la kaunti.
Akifika mbele ya kamati hiyo Esther Chelimo ambaye amependekezwa kuhudumu katika wizara ya ardhi, nyumba mipangilio na maendeleo ya miji, amesema kwamba japo kuna changamoto nyingi kuhusiana na maswala ya ardhi kaunti hii, atatumia nafasi hiyo kuwaelimisha wakazi kuhusu umuhimu wa sheria katika kusuluhisha maswala ya ardhi.
Kwa upande wake Wilfred Longronyang aliyependekezwa kuhudumu katika wizara ya kilimo, mifugo na uvuvi amesema kuwa wizara yake itahakikisha kwamba wakulima wananufaika pakubwa na shughuli za kilimo kwa kukifanya kuegemea zaidi mapato.
Rebecca kibe aliyependekezwa kuhudumu kama waziri wa elimu aliihakikishia kamati hiyo kuwa atajitolea kuhakikisha idara ya elimu inaimarika chini ya utawala wake wakati uo huo akishirikiana na gavana wa kaunti hii kufanikisha manifesto yake kwa wakazi.
Aidha waziri mteule wa afya Cleah chemutai aliahidi kuimarisha sekta ya afya akiwakikishia wakazi kwamba katika kipindi cha miaka mitano ijayo wataona mabadiliko makubwa katika sekta ya afya ambayo imekabiliwa na changamoyo tele katika kaunti hii.
Wengine walioteuliwa katika baraza hilo ni pamoja na Paul Loyakapel katika wizara fedha na mipango ya uchumi, lucky Chemutai Litole katika wizara ya maji mazingira na raslimali, Ruto Joshua katika wizara ya barabara na uchukuzi, Martine Aperen wizara ya huduma za umma maswala yaliyoghatuliwa na maswala ya teknolojia, William Lopewot wizara ya biashara na viwanda na Joshua Siwanyang katika wizara ya tamaduni, utalii michezo na maswala ya vijana.